Ubovu wa barabara wananchi washindwa kupata mahitaji

 


Baadhi ya wanakijiji wa kijiji cha Mnyangara Kata ya Mipingo Manispaa ya Lindi wamekosa huduma ya barabara kwa takribani wiki mbili baada ya mvua kuharibu miundombinu ya Daraja la Mto Mangoma na kushindwa kupitika.

Kutokana na changamoto hiyo, leo Machi 9, 2024 baadhi ya wanakijiji wamejitolea kutengeneza njia ya muda ili huduma ya barabara iweze kurejea kijijini hapo.

Akizungumza wakati kazi hiyo ikiendelea, mmoja wa wanakijiji amesema kwa wiki mbili wamekosa huduma muhimu kwa kutopitika kwa barabara hiyo.

"Kwa wiki mbili hatukuweza kupata huduma za kijamii nje ya kijiji chetu, kutokana na mvua kunyesha, maji yameanzisha mfereji mpya na kusababisha upande mmoja wa daraja kushindwa kupitika,” amesema.

“Baaada ya maji kupungua leo tumejitokeza wananchi kuja kutengeneza barabara ya dharura itakayosaidia kupita hata trekta, pikipiki na watembea kwa miguu tu."

Mkazi mwingine wa kijijini hapo amesema hofu yao ni kama angetokea mjamzito anayetakiwa kuwahishwa hospitalini.

"Tunaomba Serikali itusaidie itujengee hapa palipoharibika kwa sababu upatikanaji wa huduma za kijamii umekuwa mgumu na bei za bidhaa madukani zimepanda," amesema.

Akizungumzia kero hiyo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mnyangara, Ramadhani Kayoyo amesema hali sio nzuri kutokana mvua zinazoendelea kunyesha huku akiwataka wananchi wachukue tahadhari.

"Hakuna madhara yoyote yaliyotokea, leo tumeamua kuja kutengeneza njia ya dharura ili huduma za kijamii ziendelee, hata miundombinu ya daraja iko salama ni maji tu yametengeneza njia mpya na mamlaka zote zinazohusika zimepata taarifa kama watu wa Tarura (Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini) na jana walikuwa wanakuja huku wakashindwa kutokana na kujaa maji Namagutu," amesema.


Diwani wa Mipigo, Sefu Njema amekiri kuwapo kwa tatizo la barabara kutokupitika kutokana  mvua kunyesha na kuharibu miundombinu hiyo.

"Sio daraja tu kwa jumla barabara yote hali yake ni mbaya," amesema Njema.

Pia, amesema barabara hiyo ilishatengewa bajeti ya mwaka 2023/24 ya  Sh95 milioni kwa ajili ya ukarabati na mkandarasi alisharipoti tangu Novemba 2023 lakini kutokana na mvua kuanza mapema ameshindwa kuanza kazi.

Previous Post Next Post